MBUNGE wa Jimbo la Arusha Mjini, Godbles Lema (Chadema), amelitaka Bunge kuvunja Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kutokana na maoni ya kambi hiyo kutosikilizwa. Aidha, Lema amedai kuna kuchujwa kwa maneno yanayochangiwa na wabunge wa kambi hiyo katika mijadala katika taarifa za kumbukumbu za Bunge(hansard), alikodai kunafanywa na wafanyakazi wa Studio ya Bunge. Aliyasema hayo bungeni mjini hapa jana asubuhi aliposimama na kuomba mwongozo wa Kiti cha Spika akidai kuwa michango ya Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni imekuwa ikihaririwa na baadhi ya maneno yamekuwa yakiondolewa na hivyo kutorushwa kwenye studio hiyo na hata kwenye taarifa wanazopewa waandishi wa habari wa redio na televisheni. Hata hivyo, katika mwongozo wake kuhusu suala hilo muda mfupi kabla ya kuahirisha shughuli za Bunge jana mchana, Mwenyekiti wa Bunge, Najma Murtaza Giga, aliyekuwa akiongoza kikao cha jana, alisema Studio ya Bunge haina utaratibu wa kuchuja michango ya wapinzani isipokuwa kwa maelekezo ya Kiti cha Sp...